Jumatano 7 Oktoba 2026 - 02:00
Arbaeen Nchini Nigeria Imegeuka Kuwa Sehemu ya Maisha na Malezi ya Kizazi Kinachohimili Changamoto

Hawza/ Fatima Siddiqa Glima amesema: Arbaeen nchini Nigeria, licha ya uhaba wa vifaa na huduma pamoja na hatari za kiusalama, imekuwa sehemu ya mtindo wa maisha ya familia, na ushiriki wa watoto katika njia hii, kupitia kushuhudia kujitolea, mshikamano na uimara wa familia, unawapa fursa ya kuifahamu kwa vitendo dhana ya mapambano ya kusimamia misingi, uwajibikaji na utamaduni wa Ashura.

Kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza mjini Tehran, Fatima Siddiqa Glima, mwanaharakati wa Arbaeen nchini Nigeria na mwanafunzi wa udaktari, siku ya Jumatatu alizungumza katika kikao cha awali cha Mkutano wa Kimataifa wa “Arbaeen ya Husseini na Wajibu wa Kinabii”, wenye mada “Arbaeen, Mjadala wa Upinzani”, uliofanyika katika Ukumbi wa Majadiliano wa Chuo Kikuu cha Allameh Tabataba’i. Akirejea uzoefu wa familia za Nigeria katika kuandaa matembezi ya Arbaeen, alisema: Nchini Nigeria, Harakati ya Kiislamu ya Nigeria inayoongozwa na Sheikh Zakzaky imekuwa ikiandaa matembezi ya Arbaeen kwa miaka mingi, na hafla hii hufanyika kwa ushiriki mkubwa wa watu kutoka majimbo mbalimbali.

Aliongeza: Washiriki wanaotoka maeneo ya mbali huanza safari yao siku kadhaa kabla na kufika katika eneo la mkusanyiko wa Mashia nchini Nigeria siku ya Arbaeen, ili kushiriki katika maombolezo na ziara ya kiishara ya bendera ya Sayyidush-Shuhadaa (as).

Arbaeen nchini Nigeria; Safari Inayofanywa kwa Vifaa na Huduma Chache

Mwanaharakati huyo wa Arbaeen nchini Nigeria, huku akizungumzia tofauti kati ya mazingira ya matembezi ya Arbaeen nchini humo na yale ya Iraq, alisema: Katika safari hii, hakuna huduma nyingi na mawakibu ambazo mazuwari huzipata nchini Iraq, na familia zinapaswa kujiandalia mahitaji yao mengi kabla ya kuanza safari.

Glima aliendelea kusema: Familia huandaa chakula na vifaa vinavyohitajika siku kadhaa kabla ya kuanza safari, si kwa ajili yao wenyewe tu, bali pia kwa ajili ya kuwasaidia mazuwari wengine, na licha ya ugumu wa njia, huanza safari yao.

Akisimulia kumbukumbu moja kutoka utotoni mwake, alisema: Nilipokuwa mtoto na kuchoka katika njia ya Arbaeen, ndugu zangu walinibeba kwa zamu mabegani mwao ili niweze kuendelea na safari. Matukio haya rahisi huunda sehemu muhimu ya kumbukumbu na malezi ya Arbaeen kwa watoto wa familia za Nigeria.

Mazuwari wa Nigeria; Katika Njia ya Arbaeen Wakiwa na Uwezekano wa Kuuawa Kishahidi

Glima, huku akizungumzia mazingira ya kiusalama yanayotawala katika matembezi ya Mashia nchini Nigeria, alisisitiza: Kwa familia zetu, kushiriki katika matembezi ya Arbaeen si safari ya kiibada pekee; bali ni harakati inayoweza kuambatana na hatari, kujeruhiwa, kutekwa na hata kuuawa kishahidi.

Aliongeza: Mwanamume na mwanamke, na hata mtoto anayeaondoka nyumbani ili kushiriki katika hafla ya Arbaeen, anaweza kukumbana na swali la iwapo atarejea tena nyumbani au la. Mama pia anaweza kumsindikiza mtoto wake akiwa na hofu kwamba huenda asimwone tena.

Mwanaharakati huyo wa Arbaeen nchini Nigeria, huku akizungumzia kuuwawa kishahidi baadhi ya wanafamilia wake, alisema: Familia yangu pia imeathiriwa na matukio haya, na baadhi ya ndugu zangu waliuwawa kishahidi katika matukio yanayohusiana na Mashia nchini Nigeria, huku mama yangu naye akijeruhiwa na kupata ulemavu kutokana na janga la Zaria.

Aliongeza: Familia nyingi za Nigeria zina kumbukumbu chungu na nzito kutokana na matukio haya, na licha ya matatizo yote hayo, zimeendelea kudumisha uhusiano wao na utamaduni wa Ashura na Arbaeen.

Arbaeen; Uzoefu wa Kwanza wa Vitendo wa Kustahimili Changamoto kwa Watoto

Glima, akieleza kwamba mada ya hotuba yake ni “Familia ya Arbaeen”, alisema: Uzoefu halisi wa familia za Nigeria kuhusu Arbaeen unatofautiana kwa kiasi kikubwa na yale yanayoshuhudiwa katika nchi nyingine; lakini mwishowe, msingi wa harakati hii ni upendo kwa Sayyidush-Shuhadaa (as) na utamaduni wa Ashura.

Aliendelea kusema: Huenda mtoto wa miaka mitano au sita anayeshiriki katika njia ya Arbaeen kwa mara ya kwanza asiwe na ufahamu kamili kuhusu Imam Hussein (as) na tukio la Karbala; huenda kitu pekee kitakachobaki akilini mwake ni mkono wa mama yake aliokuwa ameushika au baba aliyembeba katika sehemu fulani ya safari.

Mwanafunzi huyo wa udaktari aliongeza: Lakini kurudiwa uzoefu huu kwa miaka mingi, sambamba na kushuhudia mshikamano, kujitolea na kusimama imara kwa familia, hatua kwa hatua huleta athari kubwa katika akili na haiba ya mtoto.

Glima alisisitiza: Mbegu za kwanza za vitendo za kustahimili na kupambana kwa ajili ya misingi zinaweza kuota katika moyo wa mtoto wa Nigeria katika njia hii; si kwa njia ya mihadhara na mafunzo ya moja kwa moja pekee, bali kupitia uzoefu na kushuhudia mwenendo wa familia na jamii.

Arbaeen; Shule ya Uwajibikaji na Kustahimili Changamoto

Alizungumzia athari za kielimu na kimalezi za ushiriki wa watoto na vijana katika matembezi ya Arbaeen, akasema: Kijana ambaye kila mwaka hupitia ugumu wa njia hii, hatua kwa hatua hujifunza kwamba kustahimili changamoto si kung’ang’ania tu jambo fulani analolitaka; bali kunaweza kumaanisha kuhifadhi imani katika mazingira magumu, kukubali uwajibikaji na kusimama imara mbele ya matatizo.

Glima aliendelea kusema: Katika uzoefu wa familia za Nigeria, tunaona kwa uwazi kwamba kushiriki katika njia hii kunaweza kuathiri uwajibikaji wa watu katika maisha yao, masomo yao na mustakabali wao wa kikazi.

Aliongeza: Vijana wengi wa Nigeria, licha ya kukabiliwa na matatizo mengi, wanajitahidi kusoma na kujenga mustakabali wao, na uzoefu wa miaka yao ya kushiriki katika matembezi ya Arbaeen umewafundisha kutokata tamaa mbele ya matatizo.

Mwanaharakati huyo wa Arbaeen nchini Nigeria alibainisha: Familia ambazo zenyewe zimepitia ugumu wa njia ya Arbaeen, hujitahidi kuwashirikisha pia watoto wao, ili pamoja na kuwafahamisha kuhusu Imam Hussein (as) na tukio la Karbala, wajifunze kwa vitendo maana ya kustahimili changamoto, uwajibikaji, mshikamano na kusimama imara.

Glima alisisitiza mwishoni: Kwa familia za Nigeria, Arbaeen si hafla tu; bali ni sehemu ya mtindo wa maisha na uzoefu wa kimalezi unaopitishwa kutoka kizazi hadi kizazi, na unaweza kuwa msingi wa kuunda kizazi chenye uwezo wa kustahimili changamoto, chenye kuwajibika na kilichoshikamana na utamaduni wa Ashura.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha